Jumanne 6 Mei 2025 - 12:51
Faida za Imamu Aliye Mafichoni

Je, nafasi ya Imamu katika mfumo wa kuwepo kwa viumbe ni ipi? Je, athari zote za uwepo wake zinategemea kudhihiri kwake? Je, yeye yupo tu kwa ajili ya kuwaongoza watu au uwepo wake ni chanzo cha baraka na athari kwa viumbe wote?

 Shirika la Habari la Hawza | yapata mamia ya miaka sasa, jamii ya wanadamu imezuiliwa kupata neema ya kudhihiri kwa Hujjah wa Mwenyezi Mungu na imekosa fursa ya kuwa katika uwepo wa uongozi wa kimungu na uimam wa maasum.

Je, kuwepo wa Hujjat wa Mwenyezi Mungu katika hali ya ghaiba, maisha yake katika maficho, na kutokuwa kwake wazi kwa watu wote kuna athari gani kwenye hii dunia na viumbe wote? Je, isingeliwezekana azaliwe karibu na kipindi cha kudhihiri kwake ili asishuhudie kipindi hiki kigumu cha ghaiba na kutengwa na watu wa duniani?

Maswali haya na yanayofanana nayo yanatokana na kutojua nafasi ya Imamu na Hujjah wa Mwenyezi Mungu.

Kwa kweli, nafasi ya Imamu katika mfumo wa kuwepo kwa viumbe ni ipi? Je, athari zote za uwepo wake zinategemea kudhihiri kwake? Je, yeye yupo tu kwa ajili ya uongozi wa watu au uwepo wake ni baraka kwa viumbe wote?

Imamu, mhimili wa uwepo

Kwa mujibu wa itikadi ya Kishia na kwa mujibu wa mafundisho ya dini, Imamu ni kiungo cha kufikisha fadhila za Mola kwa viumbe wote ulimwenguni. Katika mfumo wa kuwepo, yeye ndiye mhimili na mzunguko wa ulimwengu; na pasipo yeye, ulimwengu na mwanadamu, majini, malaika, wanyama na vitu visivyo na uhai haviwezi kudumu.

Aliulizwa Imamu Ja‘far as-Sādiq (‘alayhi as-salām) kwamba: Je, ardhi inaweza kubaki bila Imamu? Akasema:

«لَوْ بَقِیَتِ اَلْأَرْضُ بِغَیْرِ إِمَامٍ لَسَاخَتْ.»

“Ikiwa ardhi itabaki bila Imamu, basi itazama (na utaratibu wake utavurugika).” (Kāfī, jz. 1, uk. 179)

Hii inamaanisha kwamba Imamu (‘alayhi as-salām) ni kiungo cha kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa watu na kuwaongoza kuelekea ukamilifu wa kibinadamu ni jambo lililo wazi kabisa; kwani tangu mwanzo, Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaongoza wanadamu kupitia kwa Manabii na kisha kwa mawasii wao. Lakini kutokana na maneno ya maasumīn (a.s) inaeleweka kuwa uwepo wa Maimamu katika ulimwengu ni kama kiungo cha kupokea kila neema na fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kila kiumbe, mdogo au mkubwa.

Kwa maneno yaliyo wazi zaidi: viumbe wote wanapokea neema na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia kwa Imamu. Uwepo wao wenyewe unatokana na Imamu, vivyo hivyo neema na manufaa mengine wanayoyapata katika maisha yao yote yanatoka kwake.

Katika sehemu ya "Ziyārat Jāmi‘a Kabīrah", ambayo ni mkusanyiko wa elimu ya Ma‘arifa ya Maimamu imeandikwa hivi:

«بِکُمْ فَتَحَ اللّهُ وَبِکُمْ یخْتِمْ وَبِکُمْ ینَزِّلُ الغَیثَ وَبِکُمْ یمسِکُ السَّماءَ اَنْ تَقَعَ عَلَی الاَرضِ اِلاّ بِاِذنِهِ.»

"Enyi Maimamu wakubwa, Mwenyezi Mungu alianza kuumba ulimwengu kwa sababu yenu, na kwa ajili yenu pia atauhitimisha. Kwa ajili yenu Anateremsha mvua, na kwa baraka ya kuwepo kwenu Anazuia mbingu isishuke juu ya ardhi, isipokuwa kwa idhini Yake".

Hivyo basi, athari za uwepo wa Imamu hazijafungika tu kwenye kudhihiri kwake, bali hata akiwa katika ghaiba na maisha ya maficho, bado ni chanzo cha uhai wa viumbe wote wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu Mwenyewe ametaka kwamba Yule aliye mkamilifu zaidi awe ndiye kiungo cha kupokea na kufikisha fadhila Zake kwa viumbe wengine, na katika jambo hili hakuna tofauti baina ya ghaiba na kudhihiri kwake. Naam, wote hunufaika na athari za uwepo wa Imamu, na ghaiba ya Imamu Mahdi (‘alayhi as-salām) haileti doa lolote katika jambo hili.

Cha kuvutia ni kwamba, pale Imamu Mahdi (‘alayhi as-salām) alipoulizwa kuhusu namna ya kunufaika naye katika zama za ghaiba, alisema:

«وَ أَمَّا وَجْهُ اَلاِنْتِفَاعِ بِی فِی غَیْبَتِی فَکَالاِنْتِفَاعِ بِالشَّمْسِ إِذَا غَیَّبَتْهَا عَنِ اَلْأَبْصَارِ اَلسَّحَابُ وَ إِنِّی لَأَمَانٌ لِأَهْلِ اَلْأَرْضِ کَمَا أَنَّ اَلنُّجُومَ أَمَانٌ لِأَهْلِ اَلسَّمَاءِ.»

“Ama namna ya kunufaika nami katika ghaiba yangu ni kama kunufaika na jua ambalo mawingu yamelificha machoni mwa watu. Na hakika mimi ni amani kwa watu wa ardhini kama vile nyota zilivyo amani kwa watu wa mbinguni.” (Kamāl ad-Dīn, jz. 2, uk. 483)

Utafiti huu unaendelea…

Imenukuliwa kutoka katika kitabu “Negin-e Āfarinish” huku ikifanyiwa marekebisho kiasi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha